TANGAZO

TANGAZO

TANZANIA YASISITIZA KUIMARISHA JUHUDI ZA KUOKOA MAISHA YA MAMA NA MTOTO AFRIKA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za pamoja za kuokoa maisha ya kina mama, watoto wachanga, watoto na vijana barani Afrika, akieleza kuwa uwekezaji katika huduma bora za afya ni msingi muhimu wa kujenga familia zenye afya na mustakabali bora wa Bara la Afrika.





Akizungumza kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amesema Afrika imepiga hatua katika kupunguza vifo vya kina mama na watoto, lakini mafanikio hayo yanahitaji kulindwa na kuendelezwa kutokana na changamoto za upatikanaji wa rasilimali na mahitaji yanayoongezeka katika mifumo ya afya.


Mhe. Kombo ameyasema hayo 21 Septemba 2026 jijini New York, Marekani, wakati akizungumza katika mjadala wa ngazi ya juu ulioandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mhe. John Dramani Mahama, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa (UNGA 81), uliokuwa na kaulimbiu “Marekebisho ya Accra: Kukamilisha Mzunguko kwa Kuhuisha Mfumo wa Maendeleo ya Kimataifa.”









Waziri Kombo amesema Afrika inaandaa Mpango wa Bara wa Kuokoa Maisha ya Mama na Mtoto, utakaoweka malengo yanayopimika na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji katika juhudi za kuboresha afya ya mama, mtoto mchanga, mtoto na vijana. Kupitia kaulimbiu “Mother Africa Calls,” ametoa wito kwa Serikali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi kuendelea kushirikiana na Afrika katika kuhakikisha kuwa juhudi za kuokoa maisha zinawekewa rasilimali na kutekelezwa kwa ufanisi.


Kwa upande wake, Rais wa Ghana, Mhe. Mahama, amesisitiza umuhimu wa nchi za kusini (The Global South) kujenga uwezo wa ndani, kuimarisha mifumo ya afya na kuongeza uzalishaji wa bidhaa muhimu, ikiwemo dawa.


Aidha, Rais Mahama amempongeza Rais Samia kwa uongozi wake katika Mother Africa Initiative, akisema mpango huo unaunganisha sera za umma na uwajibikaji wa sekta binafsi katika kuimarisha afya ya mama na mtoto.