TANGAZO

TANGAZO

WAZIRI KOMBO ASISITIZA USHIRIKI WA WANAWAKE KATIKA AMANI YA MAZIWA MAKUU




 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amesema ushiriki wa wanawake katika michakato ya amani ni muhimu katika kupata suluhisho endelevu kwa changamoto za usalama katika eneo la Maziwa Makuu, hususan Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).





Mhe. Kombo amesema hayo katika Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu kuendeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama katika juhudi za amani eneo la Maziwa Makuu, uliofanyika pembezoni mwa Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani.


Amesema hali ya usalama Mashariki mwa DRC inaendelea kuwa ya kutia wasiwasi, huku wanawake na wasichana wakikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kuhama makazi, ukatili wa kingono na ukosefu wa mahitaji muhimu. Kwa msingi huo, Tanzania imesisitiza utekelezaji wa Azimio la 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza ushiriki wa wanawake katika michakato ya amani.


Mhe. Kombo amesema Tanzania imeandaa Mpango wa Kwanza wa Kitaifa wa Wanawake, Amani na Usalama wa 2025–2029, uliozinduliwa Agosti 19, 2025, unaolenga kuongeza ushiriki na uongozi wa wanawake katika amani na usalama, pamoja na kuimarisha ulinzi na mifumo ya urejeshaji inayozingatia jinsia.


Aidha, amesema Tanzania itaendelea kushiriki juhudi za kikanda kupitia ICGLR, ikiwemo Mpango wa Kikanda wa Kizazi cha Pili na Mkakati wa Upatanishi na Uratibu unaozingatia jinsia, huku ikiendelea kushirikiana na nchi za Maziwa Makuu katika kujenga amani na utulivu wa kudumu.


Kwa upande wake, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Afrika kuhusu Wanawake, Amani na Usalama, Mhe. Balozi Liberata Mulamula, amesema wanawake hawapaswi kuishia kushirikishwa katika michakato ya amani, bali wanapaswa kupewa nafasi, mamlaka na msaada wa kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayounda amani.