Wanawake wametakiwa kujijali na kuthamini afya zao kwa kupima mara kwa mara ili kuepusha athari na madhara zaidi yanayotokana na kuchelewa kugundua ugonjwa mapema.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Florence Samizi wakati akizindua Taasisi ya Mariam Mungula Foundation inayojihusisha na masuala ya afya ya wanawake.
"Tusijisahau kina mama, tujikumbuke kwa kujali afya zetu tujitunze ili tuishi maisha marefu kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwamo saratani.
"Ukiona umefika miaka 35 kabla hujaenda kukata keki kusherehekea birthday (siku ya kuzaliwa) nenda kachunguze mlango wako wa kizazi na matiti bado yako salama, kila mwaka fanya hivyo ukishapima hivyo vitu ndiyo ukale keki ya birthday mkumbushe na mwenzio.
"Tunavyo vifaa vya kuchunguza saratani mapema mno kupotia uwekezaji uliofanywa na serikali. Tufanye hivyo kwa sababu tayari elimu mmeisikia na mtaendelea kuisikia kupitia Mariam Mungula Foundation," amesema Dk. Samizi.
Awali akizungumia Taasisi ya Mariam Mungula Foundation, Mkurugenzi na Muasisi wa taasisi hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Mungula amesema taasisi hiyo imejikita katika kutoa elimu na kuongeza uelewa kuhusu masuala muhimu yanayowagusa wanawake katika hatua mbalimbali za maosha yao ikiwamo afya ya homoni na kipindi cha ukomo wa hedhi (menopause), afya ya akili, saratani ya mlango wa kizazi, virusi vya ukimwi na uwezeshaji wanawake kiuchumi na ujasiriamali.
"Kupitia foundation hii tunataka kuvunja ukimya. Tunataka mwanamke ambaye anaingia kwenye menopause asione aibu kuzungumza kuhusu mabadiliko anayopitia. Tunataka mwanamke anayepitia changamoto za afya ya akili ajue kwamba kuomba msaada si udhaifu.
"Foundation hii imeanzishwa kwa kuamini kwamba afya ya mwanamke ni msingi wa afya ya familia na maendeleo ya jamii. Mara nyingi wanawake tunatumia nguvu nyingi kuwahudumia watoto, familia, waume, wazazi, kazi na jamii zetu lakini wakati mwingine tunasahau kujihudumia sisi wenyewe. Ndiyo maana tunataka kujenga utamaduni ambao mwanamke anaweza kusema nina haki ya kujua kinachoendelea katika mwili wangu, nina haki ya kuuliza, nina haki ya kuwa na afya njema na nina haki ya kupata huduma," amesema Mariam.
Pamoja na mambo mengine, Mariam amesema anaamini huo ni mwanzo mzuri wa safari kubwa ya kumuweka mwanamke nafasi anayostahili akiwa na uelewa, nguvu na fursa.
