TANGAZO

TANGAZO

DCP LYIMO AHIMIZA MIRADI YENYE TIJA KWA WANACHAMA WA MTANDAO WA WANAWAKE

 


Mwenyekiti wa Mtandao wa wanawake wa Jeshi la Magereza, Naibu Kamishna wa Magereza (DCP) Lipina Lyimo, leo Novemba 4, 2026, ameongoza kikao cha majumuisho ya tathmini ya Mkutano Mkuu wa Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza, kilichowakutanisha washiriki kutoka Mkoa wa Dodoma. Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Msalato, jijini Dodoma.





Akizungumza katika kikao hicho, DCP Lyimo amewashauri wanawake hao kupendekeza miradi yenye tija itakayoongeza thamani ya michango ya wanachama wa mtandao huo. Aidha, ameitaka Sekretarieti kupokea na kufanyia kazi maoni ya wanachama ili kuwezesha tathmini, majumuisho na maandalizi bora ya mkutano mkuu ujao.






Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Edith Mbogo amewataka washiriki kuzingatia usalama na faragha zao kwa kuepuka kurekodi na kusambaza picha binafsi kwenye mitandao ya kijamii. Ushauri huo ameutoa akishirikisha uzoefu alioupata wakati wa kuhudhuria mafunzo ya uongozi nchini Indonesia.


Naye Mhandisi wa Jeshi la Magereza, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP) Bonaza Malata, amewasilisha taarifa kuhusu mafunzo ya uongozi yaliyowashirikisha viongozi wanawake wanane kutoka Jeshi la Magereza, yaliyofanyika katika Shule ya  Uongozi Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha kwa Mfipa Pwani


Mafunzo hayo yalijikita katika maeneo mbalimbali, yakiwemo uongozi binafsi na kitaasisi, usimamizi wa rasilimali watu, uongozi wa kimkakati, utatuzi wa migogoro, usimamizi wa miradi, mawasiliano, matumizi ya Akili Mnemba (AI), teknolojia za kidijitali, usalama wa taarifa na uwezeshaji wa wanawake katika uongozi.


Akitoa ufafanuzi kuhusu uendeshaji wa mtandao huo, Katibu wa Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza, INSP Scholastica Ndunguru, amesema mtandao una Katiba inayoweka mwongozo wa uendeshaji wa vikao na mikutano mbalimbali. Aidha, amewahimiza wanachama kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu ya mtandao huo.


Amesema mtandao huo ulianzishwa mwaka 2018 ukiwa na malengo mbalimbali, ikiwemo kuongeza uelewa wa wanawake kuhusu masuala yanayohusu mazingira yao ya kazi, pamoja na kusimamia haki na stahiki za makundi maalumu ya wahalifu wa kike, wakiwemo wajawazito, wanawake wenye watoto na watoto walio katika mgogoro na sheria.