TANGAZO

TANGAZO

JKI Yagawia Vitimwendo, Mitaji na Chakula Wenye Ulemavu na Wajane Ilala, DC Mpogolo Aipa Tano



Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Jamii Kwanza Initiative (JKI) iliyopo Ilala, Jijini Dar es Salaam, leo Novemba 16,2026 imetoa nyenzo mbalimbali vikiwemo vitimwendo, vyerehani, mitaji na chakula kwa watu wenye ulemavu na wajane.





Akizungumza kwenye hafla fupi ya ugawaji wa nyenzo hizo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameipongeza na kuishukuru taasisi hiyo kwa jitihada zake za kuhakikisha watu hao wanapata mahitaji muhimu yatakayowawezesha kuendesha maisha yao.


"Hongereni kwa kuzifanya hizi familia kupata uhuru wa kuendelea na kazi zao, hasa wakinamama huku wakilea watoto wao."


Mpogolo ametoa wito kwa viongozi na wadau mbalimbali kujitokeza na kuiunga mkono Serikali na taasisi hiyo kwa kuwasaidia wakinamama kiuchumi ili wasiwe tegemezi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKI, Daniel Migera, ameeleza kuwa taasisi imeamua kutimiza ahadi yake kwa kugawa vitimwendo kwa watoto wenye ulemavu waliokosa awamu ya kwanza, pamoja na vyerehani na mitaji kwa wakinamama hao ili walee familia na kuendesha maisha yao.


"Tunatoa tena leo kwa sababu ni ahadi na imani, na lengo ni kugusa maisha ya wenye uhitaji na ni sadaka bora."


Migera ameipongeza na kuishukuru Taasisi ya "Tumaini Pamoja Nasi" iliyoanzishwa kwa ajili ya kuwaweka pamoja watu wenye watoto walemavu ili wapate kusaidika kwa pamoja.


Jamii Kwanza Initiative ni taasisi isiyo ya Kiserikali inayojihusisha na kusaidia wenye uhitaji, kuweka mipango inayolenga kuboresha elimu, upatikanaji wa maji safi na salama, na uwezeshaji wa kijamii kupitia haki za kijinsia, fursa za kiuchumi, na maendeleo ya uongozi.