TANGAZO

TANGAZO

PROF. KABUDI ATANGAZA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI 2026, ASILIMIA 95 WATAMBULIWA HALI ZAO



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ametangaza maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani 2026 ni kuanzia tarehe 24 Novemba hadi 1 katika Kanda zote saba za TACAIDS.




Prof. Kabudi ameyasema hayo leo Novemba 19, 2026 katika Mkutano wake na Waandishi wa habari Jijini Dar Es salaam amesema kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika tarehe 1 Desemba 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Convention Centre, Dodoma, ambapo pia kutafanyika Jubilei ya Miaka 25 ya TACAIDS.



Mgeni rasmi katika kilele hicho anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.

Prof. Kabudi amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI na imefanikiwa kufikia malengo ya 95.

Amesema asilimia 95 ya watu walio na VVU wametambua hali zao, asilimia 95 ya wale wanaotambua kuwa wanaishi na VVU wanatumia dawa za ARV, na asilimia 95 ya wale wanaotumia ARV wamefubaza VVU mwilini.

Ameongeza kuwa hadi Desemba 2025, asilimia 92.7 ya watu wanaoishi na VVU wamepima na kutambua hali zao, asilimia 99.5 wanapata huduma ya ARV na asilimia 98.2 wamefubaza VVU.

Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, maambukizi mapya ya VVU yamepungua kutoka watu 98,754 mwaka 2010 hadi watu 33,511 mwaka 2025, huku vifo vitokanavyo na UKIMWI vikishuka kutoka watu 55,833 hadi watu 25,995.

Amesema pia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua kutoka asilimia 9.1 hadi asilimia 6.2.

Utafiti wa Tanzania HIV Impact Survey (THIS) wa mwaka 2022/23 unaonesha kuwa Tanzania Bara ina watu 1,690,948 wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15 hadi 49, kati yao watu 1,559,154 wanatumia dawa za ARV.

Prof. Kabudi ametoa wito kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, ambao wanachangia asilimia 33.3 ya maambukizi mapya, kujikinga, kujua hali zao na kushiriki kutoa elimu sahihi kwa jamii.

Amesema kati ya vijana hao, asilimia 77.7 ya maambukizi mapya yapo miongoni mwa vijana wa kike.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji wa rasilimali za ndani, kuhamasisha sekta binafsi na kuendeleza ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha huduma za kinga, upimaji na matibabu zinaendelea kupatikana.

Amehitimisha kwa kusema jukumu la mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ni la kila mmoja, na akatoa wito wa kushirikiana kujenga jamii yenye uelewa kuhusu VVU na UKIMWI isiyo na unyanyapaa.

Ametoa wito kwa wananchi katika Kanda za Kaskazini, Kusini, Mashariki, Magharibi, Kati, Ziwa na Zanzibar kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo.