TANGAZO

TANGAZO

PROF. SHEMDOE: WATUMISHI WA UMMA NI NGUZO YA MAENDELEO, AWATAKA KUWAJIBIKA KIKAMILIFU




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema watumishi wa umma ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Lushoto, hivyo anawathamini kwa utendaji wao na mchango wao katika kuleta maendeleo ya taifa na kutoa huduma kwa wananchi.






Prof. Shemdoe ameyasema hayo leo, Novemba 20, 2026, wakati wa kikao kazi chake cha kuhimiza uwajibikaji kwa Watendaji Kata, Maafisa Tarafa, Wakuu wa Shule za Sekondari, Walimu Wakuu wa Shule za Msingi, Waganga Wafawidhi, Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizopo katika Jimbo la Lushoto.


“Ninyi ndugu zangu ndio funguo ya maendeleo hapa Lushoto, hivyo ninathamini sana kazi mnazozifanya katika kutekeleza majukumu yenu na jukumu la kuliletea taifa maendeleo,” amesisitiza Prof. Shemdoe.


Prof. Shemdoe amewataka watumishi hao kuhakikisha kila mmoja anatekeleza kikamilifu majukumu aliyokabidhiwa na Serikali kwa nafasi yake, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa upendo, umoja na ushirikiano ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake.


Aidha, amewataka watumishi hao kuhakikisha wanaporejea katika maeneo yao ya kazi wanatekeleza kwa ufanisi jukumu la kusimamia miradi ya maendeleo, ikiwemo ya elimu, afya na miundombinu ya barabara, ili ikamilike kwa wakati na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi pamoja na kuimarisha shughuli za kiuchumi.


Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amewapongeza watumishi wa umma wa Lushoto kwa utendaji kazi wao mzuri na kuwakumbusha kuwa jukumu lao kubwa ni kuwahudumia wananchi, kuwaletea maendeleo na kuwapatia tabasamu la kudumu, kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.