Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa kupitia mfuko wa dharura (CERC) imeongeza mtandao wa barabara kwa kufungua barabara mpya ya Kasisiwe-Pito yenye urefu wa Kilomita 11.4 kwa kiwango cha changarawe inayounganisha kata za Milanzi na Pito katika Manispaa ya Sumbawanga.
Ufunguaji wa barabara hiyo umewaondolea adha ya usafiri na usafirishaji wakazi vijiji vya Pito, Malagano na Tamesenga ambao walikuwa wanapitia Mlanda wakizinguka umbali wa Km 32 kuzifikia huduma za kijamii na kiuchumi katika Manispaa ya Sumbawanga.
Meneja wa TARURA wilaya ya Sumbawanga, Mhandisi Albert Kyando amesema mradi huo una jumla kilomita 11.4 ambao unahusisha kusafisha eneo, kunyanyua tuta la barabara, uwekaji wa changarawe kilomita zote 11.4 pamoja na ujenzi wa maboksi kalavati tisa (9).
Amesema kwa sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 80 na kuongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha mawasiliano kati ya eneo la Manispaa kwa maana ya Kasisiwe kata ya Milanzi na vijiji vya Pito, Malagamo na Tamesenga katika kata ya Pito.
"Vijiji hivi kwa kiasi kikubwa ndio vinalisha Mji wa Sumbawanga hasa upande wa mbogamboga lakini pia vijiji hivi ni vya wakulima kwa hiyo kukamilika kwa barabara hii kutarahisisha usafirishaji wa mazao na pembejeo za kilimo".
Kwa mujibu wa Mhandisi Kyando barabara hiyo pia itasaidia wananchi kwa sababu inapopita barabara hiyo ndipo inapojengwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa hiyo itawaunganisha wananchi na huduma za afya na elimu kupitia Chuo cha Ualimu Sumbawanga na gharama za mradi huo zinatolewa kupitia mfuko wa dharura (CERC) ambao ni mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa wa Kasisiwe Bw. Ezekiel Mwakasege amesema ujenzi wa barabara hiyo umepandisha thamani ya ardhi yao na kwamba utasaidia kuvutia wawekezaji katika maeneo yao kuwekeza hasa katika eneo la kilimo.
Bw. Mwakasege ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutawapunguzia wananchi mzunguko na gharama za usafiri kwani hapo awali walikuwa wakizinguka mpaka kijiji cha Mlanda kufika mjini Sumbawanga na walikuwa wakitumia gharama kubwa.





