Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imewapeleka nchini Afrika Kusini watumishi wake wanne kupata mafunzo ya wiki moja kuhusiana na Uhifadhi wa faru katika hifadhi ya Phinda Private game Reserve iliyopo Kwazulu Natal.
Mafunzo hayo yanatokana na ushirikiano wa karibu uliopo baina ya Hifadhi ya Ngorongoro na Phinda private Game Reserve ambapo hifadhi hizi zimekuwa zikishirikiana katika kufanikisha kuwalinda wanyama hao.
![]() |
Kiongozi wa Ujumbe huo, Kanali Fikiri Machibya ambaye ni mshauri wa Jeshi la Uhifadhi ameeleza kuwa mafunzo hayo yameendelea kuwasaidia kujua mbinu ambazo hifadhi ya Phinda wanazotumia kulinda, kuhifadhi,kuzuia uharibifu, kufuatilia miendendo ya wanyamapori, mimea na matumizi ya teknolojia kama njia ya kisasa na imara kwenye ulinzi katika maeneo yenye changamoto.
Afisa Mhifadhi Mwandamizi ambaye ni mratibu wa Faru Ngorongoro Deogratius Maige ameeleza kuwa; "Ili nchi au taasisi ifanikiwe kuwahifadhi Wanyama adimu kama Faru ni muhimu kuwajengea uzoefu kwa vitendo watumishi kwenye nchi ambazo zina uzoefu mkubwa wa kuwahifadhi na kuwalinda Wanyama hao,
Mafunzo hayo pia yamekuwa ni sehemu ya kubadilishana uzoefu kuhusu uhifadhi shirikishi kwa jamii zinazozunguka hifadhi, wajibu wa kutoa kwa jamii (CSR), uchomaji moto maeneo ya hifadhi kuimarisha malisho, kudhibiti uvamizi wa mimea na utoaji wa ajira za muda mfupi na mrefu kwa jamii zinazosaidia shughuli za uhifadhi.
Hifadhi ya Wanyamapori Binafsi ya Phinda iliyopo Jimbo la KwaZulu-Natal Nchini Afrika kusini ina ukubwa wa hekta 29,866 na moja ya maajabu ya dunia ikijumuisha wanyama mbalimbali wakiwepo Big Five (simba, chui, tembo, faru na nyati) na zaidi ya spishi 436 za ndege na kuifanya kuwa moja ya maeneo yanayoongoza kwa wanyamapori wengi Afrika Kusini.





