TANGAZO

TANGAZO

AMANI NA UTULIVU NDIO MSINGI: BILA UTULIVU HAKUNA VYAMA WALA BENDERA NCHINI




Upendo, amani, na utulivu vimetajwa kuwa ndio kila kitu na urithi mkuu ambao kizazi cha sasa kinapaswa kuwaachia vijana, ikiwa ni kuenzi misingi imara iliyoachwa na mababu tangu enzi za kupigania uhuru. 

Evelyne Abel Mwalwisi, mkazi wa Tabata Kimanga jijini Dar es Salaam, ametoa wito mzito akisisitiza kuwa amani ndiyo inayotoa nafasi ya kuwepo kwa mambo mengine yote, ikiwemo siasa na vyama, kwani bila utulivu hakuna bendera ya chama chochote inayoweza kupepea. 

Amewaasa vijana na watoto kutokukurupuka wala kuiga mambo yasiyofaa, bali wazingatie misingi ya malezi waliyofundishwa na wazazi wao ili kuendeleza mnyororo wa amani ambao umekuwa utambulisho wa kipekee wa Tanzania.

Akielezea madhara ya vita, Mwalwisi amebainisha kuwa gharama ya kuvuruga amani ni kubwa mno na ni vigumu kuirejesha pindi inapopotea, akitolea mfano hai wa nchi jirani zinavyohangaika kutokana na machafuko. 

Amesema kuwa katika nyakati za vita, hakuna anayeangaliwa dini yake wala itikadi yake, na waathirika wakubwa daima hubaki kuwa watoto wasio na hatia, wanawake wajawazito, na watu wengine wengi wanaopoteza maisha huku damu ikimwagika bila sababu. 

Hali hiyo hupelekea hata shughuli za kijamii na kiroho kama kwenda makanisani kusimama, jambo linalopaswa kuwa funzo kwa Watanzania kutojaribu kabisa kuchezea utulivu uliopo.

Neno la faraja na husia kwa vijana limejikita katika kuitunza amani ya nchi kwa nguvu zote, kwani uhuru wa Tanzania ulipatikana kwa njia ya amani na ni wajibu wa kila mmoja kuuendeleza. 

Mwalwisi amehitimisha kwa kusema kuwa amani na upendo ni kila kitu, na vijana wanapaswa kuelewa kuwa amani ikishavurugika, hakuna cha chama wala dini kitakachobaki salama. 

Hivyo, jamii imetakiwa kuendelea kuenzi amani na utulivu kama tunu muhimu iliyoachwa na wazee, tukijifunza kupitia majanga ya wengine ili tusiweze kufika huko, bali tubaki tukiwa wamoja kwa ajili ya maendeleo ya sasa na ya baadae.

Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com