Katika kuhakikisha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa huduma bora kwa wananchi kwa kutumia vifaa vya kielektroniki pamoja na mifumo mbalimbali ya kidigitali, wananchi na wadau Mkoani humo wapongezwa kwa kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo katika kuzuia na kutokomeza uhalifu.
Hayo yamesemwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Wilbert Siwa Julai 21, 2026 wakati akipokea msaada wa "Computer" iliyotolewa na Diwani wa Kata ya Ilemi kwa ajili ya kusaidia kazi za Polisi Jamii Wilaya ya Mbeya.
"Msaada huu umekuja wakati muafaka ambapo Jeshi la Polisi nchini limejikita katika matumizi ya mifumo mbalimbali ya kidigitali katika utendaji wake wa kazi, hivyo vifaa hivi vitasaidia kuongeza ufanisi na weledi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali" alisema Kaimu Kamanda Siwa.
Aidha, Kaimu Kamanda Siwa amesema kuwa elimu inayotolewa na Polisi na Wakaguzi Kata kwa makundi mbalimbali imesaidia wananchi kujua wajibu wao na kuzaa matunda ikiwemo kupungua kwa matukio ya uhalifu na kupata misaada mbalimbali ya vitendea kazi kama hivi vilivyotolewa na Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ilemi Mhe Baraka Zambi amesema kuwa, msaada huo umetolewa kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Jeshi la Polisi na Wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya.
Aidha, Mhe Zambi amesema kuwa, kutokana na uwepo wa Polisi Jamii kwa sasa katika Kata ya Ilemi uhalifu umepungua ukilinganisha na hapo awali, vijana wameelimishwa na kubadilika na kubadili mienendo yao.
Naye, Diwani wa Kata ya Iwambi Mhe Gloria Mwamajemba maarufu Mchina amesema kuwa Polisi Kata wameleta matokeo chanya katika kuimarisha ulinzi na usalama kutokana na elimu inayotolewa pamoja na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.
Kupitia falsafa ya Polisi Jamii, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kushirikiana na wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Polisi Jamii na kupelekea kupata mafanikio chanya ikiwemo kupungua kwa uhalifu.


