Watendaji wa kata na mitaa, wenyeviti, mabalozi wa nyumba kumi pamoja na viongozi wa dini zote wa Mji wa Tunduma wametakiwa kuendelea kushirikiana katika kupambana na vitendo vya ulawiti, ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia ili kulinda usalama wa watoto na jamii kwa ujumla.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika tarehe 21 Julai 2026, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Mji wa Tunduma, Mrakibu wa Polisi Daud Nalimi, akiwa pamoja na Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Momba, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Frida, aliwataka viongozi hao kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi, hususan Polisi Kata, ili kuimarisha ulinzi wa jamii, kuzuia uhalifu na kuhakikisha wahalifu wa vitendo vya ukatili wa kijinsia wanachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande mkuu wa Polisi jamii wilaya ya Momba amewahimiza viongozi hao kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, kuripoti matukio ya ukatili kwa wakati na kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi ili kutokomeza kabisa vitendo vya ulawiti, ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia katika Mji wa Tunduma.

