TANGAZO

TANGAZO

ASKARI WANAFUNZI 1,561 KUKAMILISHA MAFUNZO YA MIEZI TISA KIWIRA

 



Askari wanafunzi 1,561 wa Jeshi la Magereza wanatarajiwa kuhitimu mafunzo ya awali ya Kozi Na. 33 baada ya kukamilisha mafunzo yaliyodumu kwa takribani miezi tisa katika Chuo cha Magereza Kiwira, jijini Mbeya.





Kati yao, wanawake ni 367 na wanaume 1,194. Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea weledi na nidhamu, pamoja na kuwaandaa kutekeleza majukumu yao ya kiutumishi kwa kuzingatia misingi na taratibu za Jeshi la Magereza.




Hafla ya kuhitimisha mafunzo hayo inatarajiwa kuongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Franklin Jasson Rwezimula ambaye pia anatarajiwa kuzindua nyumba tatu za makazi ya askari zilizopo chuoni hapo.


Nyumba hizo zina uwezo wa kuhudumia jumla ya familia sita za askari, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa makazi kwa watumishi na kuimarisha mazingira ya huduma katika Chuo cha Magereza Kiwira.

 

Katika mazoezi ya mwisho ya maandalizi ya hafla hiyo, walikuwepo viongozi waandamizi wa Jeshi la Magereza, akiwemo SACP Amani Mwinja, SACP Joe Matani, SACP Elizabeth Mbezi, SACP Keneth Mwambije na Mkuu wa Chuo cha Magereza Kiwira, ACP Fred Wambura, pamoja na maafisa na askari wengine.