TANGAZO

TANGAZO

AFRIKA YAWEKA MKAKATI WA MIAKA 20 KUIOKOA BIASHARA YA ALMASI



-Dkt. Kiruswa asema umoja na uongezaji thamani ni nguzo za ushindani wa almasi za Afrika duniani

-Nchi wanachama wa ADPA zakubaliana na dira ya “Ngoma Tano, Dira Moja, Sauti Moja”

Umoja wa Nchi Wanachama wa Chama cha Nchi za Afrika Zinazozalisha Almasi (ADPA) umekubaliana kuweka mkakati wa pamoja wa miaka 20 ijayo wa kuimarisha biashara ya almasi barani humo, kukabiliana na changamoto ya kushuka kwa bei katika soko la dunia na kuongeza thamani ya rasilimali hiyo ndani ya Afrika.





Mkakati huo, uliopewa jina la “Ngoma Tano, Dira Moja, Sauti Moja,” umelenga kuimarisha ADPA katika kuitangaza na kuilinda biashara ya almasi asilia, hasa katika kipindi ambacho sekta hiyo inakabiliwa na ushindani unaochochewa na almasi zinazozalishwa kwa teknolojia ya maabara.


Akizungumza jijini Luanda, Angola, wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya ADPA, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuimarisha umoja, ushirikiano na kuwa na msimamo wa pamoja katika kulinda na kuendeleza maslahi ya sekta ya almasi katika soko la kimataifa na kwamba maadhimisho hayo ni fursa ya kutathmini mafanikio na changamoto za sekta hiyo, pamoja na kuweka msingi imara wa maendeleo yake katika miongo miwili ijayo.




Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa ADPA ilianza safari yake ya kihistoria Novemba 4, 2006, kupitia kusainiwa kwa Tamko la Luanda, lililoweka msingi wa kuanzishwa kwa chama hicho na kubainisha kuwa katika kipindi cha miaka 20, ADPA imekuwa jukwaa muhimu la kuunganisha nchi zinazozalisha almasi, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za sekta hiyo duniani.


Amesisitiza kuwa katika miaka 20 ijayo, Afrika inapaswa kwenda zaidi ya kuzalisha na kuuza almasi ghafi kwa kuongeza uwekezaji katika teknolojia, ukataji na ung’arishaji wa almasi, utengenezaji wa bidhaa za usonara na kuimarisha ushiriki wa nchi za Afrika katika biashara na masoko ya kimataifa na kuwa kuwa uongezaji thamani ndani ya bara hilo ni muhimu katika kukuza viwanda, kuongeza ajira, kuhamisha teknolojia na kuhakikisha rasilimali za almasi zinachangia maendeleo ya wananchi.


Akifafanua dira ya “Ngoma Tano, Dira Moja, Sauti Moja,” Dkt. Kiruswa amesema nguzo zake tano ni kuwa na sauti moja katika kutetea maslahi ya Afrika, kuweka viwango vya pamoja vya uzalishaji endelevu, kuimarisha soko na imani ya walaji katika almasi asilia, kuboresha upatikanaji wa taarifa na utaalamu wa masoko, pamoja na kuunganisha nguvu za nchi wanachama katika kuitangaza almasi ya Afrika kimataifa na kuthibitisha dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuiunga mkono ADPA kupitia uzalishaji endelevu, usimamizi wa sekta, tafiti za kijiolojia, maendeleo ya wataalamu na uongezaji thamani ya madini nchini.


Vilevile, ameeleza kuwa Tanzania inaunga mkono utekelezaji wa Kiwango cha Uendelevu katika Sekta ya Almasi (Sustainable Diamond Standard - SDS), akibainisha kuwa ni muhimu katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji, utunzaji wa mazingira na imani ya walaji na kusisitiza kuwa mafanikio ya sekta ya almasi hayapaswi kupimwa kwa kiasi cha almasi ghafi kinachozalishwa pekee, bali pia kwa mchango wake katika kuongeza ajira, kujenga viwanda, kuhamisha teknolojia, kukuza biashara za ndani na kuboresha maisha ya wananchi.


Dkt. Kiruswa ametoa wito kwa nchi wanachama wa ADPA kuhakikisha maazimio ya mkakati wa miaka 20 yanatekelezwa kwa vitendo na kuleta matokeo yanayopimika, akisisitiza kuwa Afrika inapaswa kutumia umoja wake kuwa nguvu ya kiuchumi na rasilimali zake za almasi kuwa kichocheo cha maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho. “Ngoma Tano, Dira Moja, Sauti Moja -Umoja wa Afrika katika Kuunda Mustakabali wa Almasi za Afrika,” ndiyo dira ambayo Tanzania inaendelea kuiunga mkono katika kuimarisha ushirikiano na maendeleo ya sekta ya almasi barani Afrika.