Madiwani wa Halmashauri za Wilaya za Mpanda na Nsimbo mkoani Katavi, wakiongozana na baadhi ya wabunge na viongozi wengine, wamepongeza uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) baada ya kujionea kwa karibu uendeshaji wa kituo hicho na mchango wake katika maendeleo ya sekta ya nishati nchini.
Viongozi hao walitembelea kituo hicho tarehe 20 Juni 2026 kwa lengo la kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali, kufahamu namna kituo kinavyoendeshwa pamoja na kupata uelewa wa mchango wake katika kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini. Ziara hiyo ilihusisha madiwani 22 pamoja na baadhi ya wabunge na viongozi wengine kutoka Mkoa wa Katavi.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda, Charles Philipo, aliishukuru Serikali kwa juhudi kubwa inazoendelea kufanya katika kuimarisha sekta ya nishati na kuipongeza TANESCO kwa kuwapatia viongozi hao fursa ya kujionea kituo hicho.
“Tunaishukuru Serikali yetu kwa namna ambavyo imejikita kutatua changamoto ya umeme. Nipende kuwashukuru TANESCO kwa niaba ya waheshimiwa madiwani wa Mpanda na Nsimbo kwa kuona namna ya sisi kuja hapa na kujionea kituo hiki,” alisema Philipo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, Mhe. Anna Mpembe, alisema ameoneshwa kuvutiwa na ukubwa wa kituo hicho na kiwango cha uwekezaji kilichowekwa katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha kwa maendeleo ya taifa.
“Leo tunaona maajabu na miujiza kupitia Kituo cha Julius Nyerere. Jinsi kilivyojengwa ni kitu cha thamani kubwa sana katika nchi yetu ya Tanzania,” alisema Mhe. Mpembe.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mpanda, Joseph Lwamba, alisema maendeleo ya sekta ya umeme yameendelea kubadilisha maisha ya wananchi kwa kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Katavi.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba katika wilaya yetu ya Mpanda karibu vijiji vyote sasa vina umeme. Wananchi wanaweza kufanya shughuli zao za maendeleo kupitia umeme huu,” alisema Lwamba.
Akielezea lengo la ziara hiyo, Mhandisi wa Usafirishaji Umeme Mkoa wa Katavi, Victor Ngw'igulu, alisema viongozi hao wameletwa katika kituo hicho ili kujionea kwa macho maendeleo makubwa yanayofanywa na Serikali kupitia sekta ya nishati na kuwa mabalozi wa kueleza wananchi mafanikio hayo.
“Wananchi wanapaswa kujua nini kinafanywa na TANESCO kupitia Wizara ya Nishati na hii ni sehemu nzuri ya kuona maendeleo yanayofanywa katika nchi yao. Kupitia Mkoa wa Katavi tumewaleta waheshimiwa hawa ili wajionee kwa macho kile walichokuwa wanakisikia kuhusu Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere, namna kinavyofanya kazi na kuchangia katika uchumi wa taifa,” alisema Ngw'igulu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere, Mhandisi Elinainyi Kalalu, alisema ujio wa viongozi hao una mchango mkubwa katika kuendelea kuhamasisha uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kituo hicho na nafasi yake katika maendeleo ya taifa.
“Tumewapitisha katika maeneo mbalimbali na kuwaonyesha miundombinu inayotumika katika uzalishaji wa umeme. Tuna imani kwamba wataichukulia ziara hii kama chachu ya maendeleo na watakuwa wajumbe wazuri huko waendako, hasa katika kuelezea mchango wa Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere katika maendeleo ya taifa,” alisema Kalalu.
Ziara hiyo imewapa madiwani wa Mpanda na Nsimbo pamoja na viongozi wengine kutoka Mkoa wa Katavi fursa ya kujionea kwa karibu uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya nishati kupitia Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere. Aidha, viongozi hao wameeleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa na kuahidi kuendelea kuhamasisha wananchi kutambua mchango wa kituo hicho katika kuimarisha upatikanaji wa umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.



