TANGAZO

TANGAZO

RC CHALAMILA AKAGUA MIUNDOMBINU YA MAJI MABWEPANDE-BUNJU




Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe Albert Chalamila, ametoa rai kwa wananchi wanaotumia maji yanayosambazwa kupitia bomba kuu la Mab­wepande–Bunju kuelekea maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kuwa wavumilivu wakati wa matengenezo makubwa ya miundombinu ya maji yanayotarajiwa kufanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).




Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea miundombinu ya maji iliyopo Mab­wepande jijini Dar es Salaam, Chalamila amesema matengenezo hayo yanahusisha uzamishaji wa bomba kubwa la maji, hatua inayoweza kusababisha kupungua kwa kasi ya upatikanaji wa maji kwa takribani siku nne hadi tano.


Amesema wananchi wanapaswa kuelewa kuwa huenda maji yasiendelee kutoka kwa kasi waliyoizoea, lakini hayatasimama kabisa, huku akieleza kuwa ni bora kuvumilia changamoto hiyo kwa siku chache ili kufanikisha matengenezo kuliko kusubiri miezi miwili hadi mitatu wakati kiwango cha maji kwenye mito kinapokuwa kimepungua.


Aidha, RC Chalamila amepongeza kazi nzuri inayofanywa na DAWASA licha ya kuwa bado maji hayapatikani kwa asilimia 100 kwa wananchi ambapo amewataka wananchi wanaodaiwa bili za maji kulipa madeni yao, huku akiwataka wanaojihusisha na wizi wa maji kuacha mara moja vitendo hivyo.