Mkuu wa Jeshi la Magereza (CGP), Jeremiah Yoram Katungu, leo Oktoba 19, 2026, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, amewavalisha vyeo Maafisa 39 wa Jeshi la Magereza, wakiwemo Naibu Makamishna 17 na Makamishna Wasaidizi Waandamizi 22, katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Msalato, jijini Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, CGP Katungu amemshukuru Rais kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Magereza kwa kujaza nafasi za uongozi, kuboresha stahiki za watumishi na kutoa vibali vya ajira. Amesema kupandishwa vyeo kwa idadi hiyo ya Maafisa ni tukio la kihistoria, huku akiahidi kuwa Jeshi litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi.
Amewataka Maafisa hao kutumia vyeo walivyopata kuongeza bidii na kusimamia majukumu ya Jeshi, ikiwemo kutoa hifadhi salama kwa wafungwa na mahabusu, kutekeleza programu za urekebu na kutoa ushauri wa kuzuia uhalifu katika jamii.
Kwa upande wake, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza (CP), Nicodemus Tenga, amewataka Maafisa hao kutafsiri mikakati na maelekezo ya Serikali kwa vitendo, huku wakizingatia Sheria,Taratibu na miongozo inayotolewa ya Jeshi.

















