TANGAZO

TANGAZO

WANANCHI HIFADHI YA NGORONGORO KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI


Wananchi wa kata za Endulen, Alaetoli na Kakesio zilizopo eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wanatarajiwa kunufaika na mradi wa maji unaotekelezwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi  ya Ngorongoro ambapo kwa kata ya Endulen kisima chenye urefu wa mita 250  chenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita za maji 80,000 kwa siku kimechimbwa katika eneo la Mlima Matiti kata ya Endulen. 




Akiwa katika ziara ya kukagua ujenzi wa mradi huo ambao utekelezaji wake upo zaidi ya 50%, Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka  ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq Badru ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia wananchi wa kata za Endulen, Alaetoli, Kakesio na baadae Olbalbal ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji kwa mifugo hasa msimu wa kiangazi.


“Hapa kata ya Endulen baada utafiti tumepata maji ya kutosha, kisima kilichochimbwa katika eneo hili kitazalisha lita 8,000 kwa saa na lita laki moja (100,000) kwa siku, tunaamini ndani ya wiki moja majaribio ya mwisho ya kujaza maji yatakuwa yamekamilika, mabwawa ya kukusanya maji yatachimbwa na mifugo zaidi ya 2000 itakuwa inapata maji hapa kila siku,” alifafanua Badru


Kamishna Badru ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo kwa ajili ya wananchi wanaoishi eneo la hifadhi ya Ngorongoro ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya kijamii ambayo wananchi waliomba Mamlaka hiyo kuwasaidia ili kukabiliana na changamoto za ukame na kuepuka kuingiza mifugo maeneo maalum ambayo hayaruhusiwi kuingiza mifugo ndani ya hifadhi. 


Baada ya kukamilika mradi wa maji kata ya Endulen, visima vingine vitachimbwa katika kata za Kakesio na Olbalbal ambapo wananchi watanufaika kwa kunweshea mifugo yao pamoja na matumizi ya Nyumba.


Mmoja wa wananchi wa Kata ya Endulen Siyapaa Ole-Keyan amesema utekelezaji wa miradi katika kata hizo Serikali imejibu kilio cha kunusuru mifugo yao hasa kipindi cha kiangazi na wao kujiepusha kupeleka mifugo yao maeneo yasiyoruhusiwa katika nyanda za misitu na eneo la Ndutu ambalo ni mazalia ya Nyumbu wanaohama.

Kama una Taarifa,Picha, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kwa simu +255 766 166 125 au Email : emmymwaipopo@gmail.com