TANGAZO

TANGAZO

SERIKALI YAWEKEZA KATIKA UJUZI, TEKNOLOJIA KUBADILI MADINI YA VITO KUWA UTAJIRI, AJIRA






-Mbibo azindua Bodi ya Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), asisitiza kuwa kitovu cha uongeza thamani madini ya vito

-Ujenzi wa jengo la ghorofa nane la TGC wafikia asilimia 21, mafunzo na vifaa vya kisasa kuimarisha uongezaji thamani wa madini nchini.

Serikali kupitia Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) imeendelea kuwekeza katika ujuzi, teknolojia na miundombinu ya Kituo hicho kwa lengo la kuongeza thamani ya madini ya vito, kukuza fursa za kiuchumi na kuweka mazingira yatakayowawezesha Watanzania kunufaika zaidi na rasilimali za madini nchini.





Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Bodi ya TGC jijini Arusha, leo Oktoba 29 2030, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amesema kituo hicho kina nafasi muhimu katika kujenga utaalamu wa ndani na kuimarisha mnyororo wa thamani wa madini ya vito na metali za thamani. Amesisitiza kuwa uwekezaji katika ujuzi na huduma za kitaalamu ni muhimu katika kuhakikisha madini yanazalisha thamani kubwa zaidi kwa taifa.






Katika kuimarisha uwezo wa kituo hicho, Mbibo amesema Serikali inaendelea kujenga jengo la ghorofa nane kwa kutumia fedha za ndani, ambalo limefikia asilimia 21 ya utekelezaji. Sambamba na hilo, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya mafunzo na huduma kupitia ununuzi wa vifaa na mashine zinazolenga kuongeza ufanisi wa shughuli za TGC.





Kupitia kituo hicho, Watanzania wanapata fursa ya mafunzo ya astashahada na stashahada, pamoja na huduma za utambuzi wa madini ya vito, utengenezaji wa bidhaa za madini, ushauri na utafiti. Uwezo huo ni muhimu katika kukuza wataalamu wanaoweza kushiriki katika hatua mbalimbali za mnyororo wa thamani wa madini, huku ukiweka msingi wa kupanua fursa za ujasiriamali na ajira katika shughuli zinazohusiana na madini ya vito.








Mbibo ameitaka Bodi mpya ya TGC, inayoongozwa na Mwenyekiti Dkt. George Mofulu, kutekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji, akisisitiza usimamizi bora wa bajeti, miradi na rasilimali za Serikali ili uwekezaji unaofanywa ulete matokeo yaliyokusudiwa. Aidha, ameitaka Bodi kuhakikisha mipango ya Kituo inaendana na vipaumbele vya Wizara ya Madini na Dira ya Maendeleo 2050.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TGC, Dkt. George Mofulu, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuiamini Bodi hiyo na kuipa dhamana ya kusimamia maendeleo ya kituo hicho, na kusema Bodi itaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu na kuelekeza juhudi zake katika kuimarisha utendaji wa TGC ili kiwe kielelezo cha uongezaji thamani wa madini ya vito katika ukanda huu na kusisitiza kuwa dhamira ya Bodi ni kuhakikisha kituo kinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya sekta ya madini kupitia utaalamu, mafunzo na huduma za kuongeza thamani ya madini.


Kaimu Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), Mhandisi Ally Maganga, amesema uongozi wa kituo hicho uko tayari kupokea na kufanyia kazi maelekezo pamoja na ushauri wa Bodi ili kuhakikisha TGC inafikia malengo yaliyokusudiwa wakati wa kuanzishwa kwake na kusisitiza kuwa ushirikiano kati ya menejimenti na Bodi utakuwa muhimu katika kuimarisha utendaji wa kituo na kukuza uongezaji thamani wa madini ya vito nchini.


Uimarishaji wa TGC unaendana na dhamira ya Serikali ya kutekeleza Mkakati wa Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri kwa vitendo. Kupitia uwekezaji katika miundombinu, teknolojia na utaalamu, Serikali inalenga kujenga msingi imara wa kuongeza thamani ya madini ya vito, kukuza shughuli za kiuchumi na kupanua fursa zitakazowawezesha Watanzania kunufaika zaidi na utajiri wa madini ya nchi yao.