Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Bruno Sunguya, amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya, wataiwezesha kwa vifaa Hospitali Kuu ya Kanda ya Kati ya Jeshi la Magereza, iliyopo Veyula jijini Dodoma, ili ianze kutoa huduma kwa jamii, akieleza kuwa hospitali hiyo ni yakimkakati kutokana na eneo ilipo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wataalamu wa Afya wa Jeshi la Magereza, leo Oktoba 21, 2026 katika Ukumbi wa Rugimbana jijini Dodoma, Profesa Sunguya, amelipongeza Jeshi kwa kuendelea kutoa huduma za Afya katika vituo vya Jeshi vilivyopo nchi nzima, pamoja na kufanya jitihada za kujenga Hospitali Kuu ya Kanda ya Kati, ambayo ujenzi wake upo katika hatua ambayo inaweza kutoa huduma.
"Niupongeze uongozi wa Jeshi la Magereza kwa kuandaa mafunzo haya, yatasidia wataalamu kujifunza ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, pia niwaahid Wizara ipo tayari kushirikiana nanyi katika eneo la mafunzo ili muendelee kuboresha utoaji wa huduma" amesema Prof. Sunguya
Aidha, Prof. Sunguya, amewataka wataalamu wa Afya wa Jeshi la Magereza, kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao, kufuata miongozo inayotolewa na Wizara ya Afya pamoja na kutoa elimu kwa Umma kuhusu magonjwa ya mlipuko ikiwemo ebola.
Akizungumza kwaniaba ya Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, CP. Nicodemus Tenga, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuliwezesha Jeshi la Magereza katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa hospitali, akieleza kuwa hospitali hizo zimekuwa zikitoa huduma si tu kwa watumishi wa Jeshi na Wafungwa, bali zimekuwa na msaada kwa jamii nzima.
Kwaupande wake, Mkuu wa Sehemu ya Afya Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Nsajigwa Mwankenja, amesema Jeshi lina wataalamu wa Afya ambao ni Maafisa na Askari zaidi ya 700 nchi nzima, huku likiendelea kufanya maboresho ya vituo vyake vya Afya kwa kutumia mapato ya ndani na wadau mbalimbali.







