TANGAZO

TANGAZO

WAZIRI MAVUNDE AZITAKA NCHI ZA AFRIKA KUACHA UTEGEMEZI WA MISAADA YA NJE KWA AJILI YA UTAFITI WA MADINI

 



-Angoza mkutano wa Mawaziri wa Afrika kujadili juu ya ugharamiaji utafiti na kuongeza thamani madini Afrika

-Atoa wito kwa nchi za Afrika kutumia mapato ya ndani kufadhili miradi ya madini, kuongeza thamani na kujenga uchumi wa viwanda

-Ataja utashi wa Rais Dkt. Samia wa kutenga Asilimia 10 ya Mapato ya Sekta ya Madini kufanya utafiti kama mfano wa kupunguza utegemezi wa wahisani.

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, ameongoza kikao cha Mawaziri wa Afrika kilichojadili namna ya kuimarisha ufadhili wa Sekta ya Madini kuanzia hatua za utafiti hadi uchakataji na usafishaji, akizitaka nchi za Afrika kuimarisha uwezo wa kutumia rasilimali na mapato ya ndani kuendeleza miradi ya kimkakati ya madini.





Kikao hicho cha ngazi ya mawaziri, kilichofanyika Oktoba 20, 2026, katika Mkutano wa Mining in Motion 2026, jijini Accra, Ghana kilijadili mada isemayo “Financing Africa’s Mineral Future- From Exploration to Refining”, inayolenga kuchunguza namna taasisi za fedha za Afrika na kimataifa zinavyoweza kuwezesha upatikanaji wa mitaji katika mnyororo mzima wa thamani wa madini.






Akiongoza majadiliano hayo, Mhe. Mavunde amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuanza kwa kutumia uwezo wake wa ndani kufadhili maendeleo ya Sekta ya Madini badala ya kutegemea zaidi ufadhili kutoka nje na kwamba utekelezaji wa mikakati ya ndani ya ufadhili unahitaji maamuzi madhubuti ya kisera, dhamira ya kisiasa na ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za fedha na sekta binafsi.


Akitoa mfano wa Tanzania, Mhe. Mavunde ameeleza kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kutenga asilimia 10 ya makusanyo yatokanayo na Sekta ya Madini kwa ajili ya utafiti wa kina wa kijiolojia, hatua inayolenga kuongeza wigo wa maeneo yanayofanyiwa utafiti na kubaini rasilimali zilizopo nchini na kubaishisha kuwa Tanzania bado ina fursa kubwa ya kuendeleza utafiti huo, ikizingatiwa kuwa takribani asilimia 16 tu ya eneo la nchi limefanyiwa utafiti wa kina


“Utashi wa kisiasa uliooneshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wa kutenga asilimia 10 ya mapato yatokanayo na Sekta ya Madini kwa ajili ya utafiti wa kina ni hatua muhimu katika kupunguza utegemezi wa fedha za wahisani na kuwezesha Tanzania kufadhili utafiti wa rasilimali zake kwa kutumia mapato ya ndani” amesema Mavunde. 

.


Aidha, Mhe. Mavunde ameeleza kikao hicho kuwa ufadhili wa Sekta ya Madini haupaswi kuishia katika utafiti na uchimbaji pekee, bali unapaswa kujumuisha ujenzi wa viwanda vya uchakataji na usafishaji wa madini na kusisitiza kuwa uwekezaji katika hatua hizo unaweza kuongeza ajira, kukuza ujuzi wa kitaalamu, kupanua shughuli za kiuchumi na kuongeza mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa za madini zilizoongezwa thamani.


Ameongeza kuwa Tanzania inaendelea kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini kupitia mfumo wa maudhui ya ndani (Local Content), unaolenga kuwawezesha wazawa kushiriki katika utoaji wa bidhaa na huduma kwa migodi, ambako katika kueleza umuhimu wa mkakati huo, ametaja hatua za kukuza uzalishaji wa ndani wa bidhaa zinazotumika migodini na kuimarisha uwezo wa Kampuni za Kitanzania kunufaika na fursa za biashara zinazotokana na sekta hiyo.


Katika mjadala huo, umuhimu wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, mifumo bunifu ya ufadhili na uwekezaji katika miundombinu ulijadiliwa kama sehemu ya kuwezesha maendeleo ya viwanda vya madini. Vilevile, ushirikiano wa kikanda na fursa zinazotokana na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) zilitajwa kuwa muhimu katika kujenga masoko mapana na minyororo ya thamani inayounganisha nchi za Afrika.


Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa mafanikio ya Sekta ya Madini barani Afrika yanahitaji dhamira ya kisiasa, uvumilivu na utekelezaji wa mikakati inayowezesha nchi kufadhili miradi yake na kuongeza thamani ya rasilimali zake na kueleza kuwa kwa kuimarisha uwezo wa ndani, kuendeleza viwanda na kushirikiana kikanda, Sekta ya Madini inaweza kuwa mhimili wa uchumi wa viwanda, ajira na maendeleo endelevu kwa wananchi wa Afrika.


Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi na Rasilimali Asili wa Ghana Mhe. Emmanuel Armah-Kofi Buah amezitaka nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za Sekta ya Madini, ikiwemo upungufu wa mitaji, miundombinu na nishati, pamoja na kuongeza thamani ya madini na kusisitiza umuhimu wa kuwa na mkakati wa pamoja utakaowezesha nchi za Afrika kutumia nguvu zake katika majadiliano ya uwekezaji, kuendeleza viwanda vya uchakataji wa madini na kulinda maslahi ya jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.